Alivaa viatu vya kuazima, hakupewa kiatu cha dhahabu: Mfungaji wa magoli mengi zaidi katika Kombe moja la Dunia

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Rekodi ya Just Fontaine ya kufunga mabao 13 katika Kombe la Dunia ni ya kuvutia. Sasa fikiria hakuwa amevaa buti zake mwenyewe.

Hakupata kiatu cha dhahabu (Golden Boot) kwa kuwa mfungaji bora wa mashindano ya 1958 - badala yake alipewa bunduki na gazeti la Uswidi kwa kuwa ni "mlega shabaha mzuri".

Tangu mwaka 1970, ni mara tatu tu ambapo mfungaji bora wa Kombe la Dunia amefunga zaidi ya mabao sita katika mashindano.

Katika mashindano ya sasa Mbappe na Messi tayari wana mabao manane, huku Erling Haaland akiwa na mabao saba na Kane na Jude Bellingham wakiwa nyuma kwa bao moja.

Bila shaka, raundi ya ziada ya mechi kwa ajili ya mashindano hayo ya timu 48 imewasaidia washambuliaji hawa, huku nchi zinazofika nusu fainali zikiwa na uhakika wa kucheza michezo minane.

Lakini hata hivyo, kwa sasa bado wako nyuma ya mchezaji aliyeweka rekodi hiyo katika mechi sita pekee.

Historia ya Fontaine

Just Fontaine alizaliwa Marrakesh Agosti 1933 - wakati huo, Morocco ilikuwa chini ya Ufaransa. Morocco ilipata uhuru miaka miwili kabla ya Kombe la Dunia la 1958, lakini kufikia wakati huo Fontaine alikuwa mchezaji maarufu wa kimataifa anayecheza katika ligi za Ufaransa - kwa hivyo aliiwakilisha Les Bleus.

Kama mwandishi wa habari za michezo na mwanahistoria Philip Barker alivyoelezea BBC Sport, Fontaine hakupangwa kuwa katika kikosi kinachoanza kwenye Kombe la Dunia nchini Sweden.

"Hakuwa chaguo la kwanza, lakini mchezaji mwenzake [Rene Bliard] aliumia katika mchezo wa kujitayarisha," anaelezea Barker. "Yalikuwa ni mabadiliko ya dakika za mwisho, ilibidi aazime buti [kutoka kwa mchezaji mwenzake Stephane Bruey] kwa mchezo wa ufunguzi kwani hakuwa na viatu vya kumtosha."

Alikuwa ameharibu viatu vyake katika kipindi cha mazoezi na hakuwa ameleta jozi ya ziada.

Akizungumza na BBC Aprili 2002, Fontaine anasema hakuwahi kufikiria kuwa mfungaji bora.

"Katika siku hizo hakukuwa na shinikizo kubwa kwetu," Fontaine alisema. "Ni waandishi wawili tu wa habari waliofuatilia timu hiyo."

"Mabosi wetu wa timu walikuwa na uhakika kwamba tungetolewa kiasi kwamba walitupa jezi tatu pekee kila mmoja, kwa hivyo tulikuwa huru kabisa hakukuwa na shinikizo."

"Akili yangu haikuwa kwenye rekodi ya mabao hata kidogo. Nilikataa hata nafasi ya kupiga penalti katika mchezo wa nafasi ya tatu!"

Katika klabu, alichezea Reims, ambayo 1957-58 ilishinda mataji mawili ya ligi na kombe la Ufaransa. Ilikuwa moja kati ya mataji manne ya Ligue 1 ambayo Fontaine alishinda - moja akiwa na klabu yake ya awali ya Nice, matatu akiwa na Reims.

Mwaka mmoja baada ya Kombe la Dunia, Fontaine alisaidia kuipeleka Reims fainali ya Kombe la Ulaya, walipoteza dhidi ya Real Madrid akiwa mfungaji bora wa mabao katika mashindano ya 1958-59 akiwa na mabao 10.

Na aliheshimiwa sana na wachezaji wenzake, akiwemo Raymond Kopa nyota wa timu ya Ufaransa ambaye alishinda Ballon d'Or ya 1958, ambapo Fontaine alishika nafasi ya tatu.

Kombe la Dunia 1958

Fontaine alifunga magoli matatu kwa Ufaransa katika ushindi wa kushangaza wa 7-3 dhidi ya Paraguay katika mchezo wa ufunguzi wa Kundi la Pili, na hilo lilimshangaza sana.

Alifunga katika kila mechi, ikiwa ni pamoja na nusu fainali, wakati Ufaransa iliposhindwa 5-2 na timu isiyozuilika ya Brazil ikiwa na Pele mwenye umri wa miaka 17.

Mchezo wa mchujo wa kusaka nafasi ya tatu ulimpa Fontaine nafasi ya mwisho ya kujaza magoli - na kufunga mabao manne katika ushindi wa 6-3 dhidi ya Ujerumani Magharibi.

Kombe la Dunia la 1958, mabao 126 yalifungwa, magoli mengi katika mashindano ya timu 16, nyuma ya mashindano ya 1954. Ufaransa ilikuwa timu iliyofunga mabao mengi zaidi, ikiwa na mabao 23.

Licha ya kuheshimiwa kama mfungaji bora wa Kombe la Dunia mwaka wa 1958, Fontaine hakuwahi kupata kiatu cha dhahabu - tuzo hiyo ilianzishwa mwaka 1982.

2014, alipewa kiatu cha kipekee cha platinamu na Fifa kwa kutambua mafanikio yake.

Kwa nini Fontaine hajulikani sana?

Jibu ni jeraha. Machi 1960, Fontaine alivunjika mguu wakati wa mchezo wa ligi ya Ufaransa. Jeraha hilo lilizidi wakati wa majaribio kadhaa ya kurudi uwanjani, kabla ya Fontaine kulazimika kustaafu mwaka 1962. Alikuwa na umri wa miaka 28 pekee.

Takwimu za mwisho za kimataifa za Fontaine: Amecheza mechi 21 kwa Ufaransa, mabao 30. Fontaine hakurudi tena kwenye Kombe la Dunia.

Baada ya kustaafu kucheza, Fontaine alibaki katika soka. Alisaidia kuunda chama cha wachezaji wa Ufaransa cha UNFP, na kuwa rais wake wa kwanza mwaka 1961.

Pia alikuwa na vipindi vya uongozi, ikiwa ni pamoja na michezo miwili akiwa meneja wa Ufaransa mwaka 1967. Baadaye alifundisha PSG na Toulouse, kabla kufundisha miaka miwili akiwa na Morocco, nchi aliyozaliwa.

"Fontaine alikuwa akitania kwamba akirudi baada ya miaka 200, rekodi yake bado ingeendelea kuwepo. Haiwezi kuvunjwa."

Fontaine alifariki tarehe 1 Machi 2023, akiwa na umri wa miaka 89. Aliona Ufaransa ikishinda Kombe la Dunia mara mbili, na kuibuka kwa Mbappe, mmoja wa wachezaji ambao wanaweza kuvunja rekodi yake.