David Beckham: Mambo matano ya kuyajua katika filamu yake ya Netflix

Iliyochapishwa

Filamu mpya ya Netflix kuhusu David Beckham imetupa ufahamu wa maisha ya mmoja wa wanasoka mashuhuri wa Kiingereza.

Upigaji wake wa mipira ya adhabu na ukataji wa nywele, Beckham alipamba kurasa za mbele na za nyuma za magazeti. Na sasa maisha yake yako katika filamu.

Filamu hiyo, iliyopewa jina la Beckham na kutayarishwa na kampuni yake ya Studio 99, inatuonyesha namna Becks alivyopanda kutoka Waltham Forest chini ya umri wa miaka 12 na kuwa na jina maarufu, pamoja na michango ya familia yake, wachezaji wenzake wa zamani na Sir Alex Ferguson.

Mapenzi na Soka

Beckham alijiunga na Manchester United ili kujifunza soka mwaka 1991, akacheza kwa mara ya kwanza katika kikosi cha kwanza mwaka uliofuata kabla ya kusaini mkataba wake wa kwanza mwaka 1993.

1996 ndipo alipojitangaza katika ulimwengu wa soka kwa kufunga kutoka katika mstari wa katikati dhidi ya Wimbledon.

Umaarufu ulifuata, lakini meneja Sir Alex Ferguson alikuwa na wasiwasi juu ya maisha yake na watu mashuhuri na uhusiano wake na mwimbaji wa Spice Girls, Victoria Adams.

Beckham anakumbuka kwamba Ferguson alitaka tu awe mwanasoka bora na kisha aoe msichana ambaye hakuwa maarufu.

Beckham alikuwa sehemu ya kikosi kilichoweka historia ya kushinda makombe matatu katika msimu wa 1999 na alishinda mataji sita ya Ligi Kuu ya Uingereza akiwa na United.

Anahusisha mafanikio hayo na "familia" yenye nguvu huko Old Trafford na katika kipindi chote cha uchezaji alimwita Ferguson kama "baba".

"Alikuwa mmoja wa watu muhimu sana katika maisha yangu tangu nikiwa na miaka 12. Ilikuwa kama familia na ndiyo sababu tulipata mafanikio ambayo tulikuwa nayo."

Kadi Nyekundu

Beckham anasema bado anajilaumu kwa kadi nyekundu ambayo alipewa wakati wakicheza dhidi ya Argentina kwenye Kombe la Dunia la 1998.

England ilipoteza mechi hiyo kwa mikwaju ya penalti, na hivyo Beckham kuwa adui namba moja wa umma.

"Natamani kungekuwa na kidonge ambacho ungeweza kunywa na kinaweza kufuta kumbukumbu," alisema. "Nilifanya kosa la kijinga na lilibadilisha maisha yangu."

"Nchi nzima ilinichukia. Popote nilipokwenda, nilinyanyaswa kila siku."

Mkewe Victoria, ambaye alikuwa mjamzito wakati huo, anamlaumu meneja wa Uingereza Glenn Hoddle kwa kuhusisha kupoteza mechi hiyo katika mahojiano yake baada ya mechi na kutolewa kwa Beckham.

Anasema kwamba Beckham "alikuwa na msongo wa mawazo na kuvunjika moyo" katika kipindi kile.

Mchezaji mwenzake wa Manchester United, Gary Neville aliongeza: "Hayakuwa sawa yaliyompata na yangemvunja moyo mwanasoka yoyote."

Mshono wa Beckham

Filamu hiyo pia inazungumzia mvutano ndani chumba cha kubadilishia nguo mwaka 2003, ambapo Ferguson alimpiga kiatu kiungo huyo.

Bosi huyo wa United alikasirika baada ya kupoteza Kombe la FA dhidi ya Arsenal, huku Beckham akitafakari: "Unapoona uso wa bosi hivi, usikae karibu naye."

Majibizano makali ya maneno kati ya wawili hao yalitokea wakati kiungo huyo alipomjibu Ferguson na kumlaani.

Albert Morgan anasema Ferguson alitembea kwa hasira huku akipiga nguo, jambo ambalo lilipelekea kiatu cha Ole Gunnar Solskjaer kuruka hewani na kumpiga Beckham.

"Lilikuwa ni tukio la ajabu," Ferguson anaeleza.

Beckham alipigwa picha akiwa na plasta juu ya jicho kufuatia tukio hilo, ingawa Ferguson alishikilia kuwa ni mguso mdogo tu na hakuhitaji kushona.

Jinamizi la Madrid

Kufuatia tetesi za kuhamia Barcelona, Beckham alisaini mkataba wa pauni milioni 24.5 na Real Madrid Julai 2003.

Hadi wakati huo uhusiano wake na Ferguson ulikuwa umeharibika. Wawili hao hawakuzungumza kamwe kuhusu uhamisho wake - jambo ambalo Beckham analitafakari kama jambo zuri kwa sababu "lingenivunja moyo" kulijadili.

Mara tu baada ya kuwasili Bernabeu, kocha msaidizi wa zamani wa Manchester United, Carlos Queiroz aliteuliwa kuwa kocha mkuu.

"Nilishtuka kwamba nilikuwa nikianza katika klabu mpya na meneja ambaye hakunitaka katika timu niliyotoka."

Nje ya uwanja, madai ya kuwa na mahusiano mengine yaliyotangazwa sana yaliathiri familia yake. Yeye na mkewe wamekuwa wakikanusha madai kwamba Beckham alikuwa na uhusiano wa kimapenzi akiwa Uhispania.

Beckham anasema ilikuwa kazi ngumu kushughulikia jambo hilo. Wapiga picha waliwafuata watoto shuleni na Victoria anakiri alichukia sana mumewe kufuatiliwa sana na vyombo vya habari.

"Ilikuwa mara ya kwanza mimi na Victoria kukumbana na jambo zito kama hilo katika ndoa yetu," anasema.

Alipenda kuwa mwanasoka

Uamuzi wa Beckham kustaafu ulikuja mapema kuliko vile alivyofikiria.

Alijiunga na klabu ya Ligue 1 ya Ufaransa Paris St-Germain Januari 2013, huku Beckham, sasa ana umri wa miaka 38, alistaafu kwa sababu akihisi kama amepigwa kila baada ya mechi.

"Nilikuwa naumwa," alisema. "Nilikuwa nikiumia. Ningetoka kitandani asubuhi kwa sababu nilikuwa na maumivu makali."

Beckham alitangaza kustaafu miezi minne baadaye na kusema "hakuweza kupumua au kudhibiti hisia zake" katika mchezo wake wa mwisho wa kulipwa.

"Niliupenda mchezo huo kuliko mtu yeyote aliyewahi kuupenda," alitabasamu. "Najua sio kweli lakini nadhani nilipenda soka kuliko mtu yeyote."