Kambi ambayo wanajeshi wa Marekani wameuawa na mashambulizi ya Iran

k

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Kambi ya kijeshi ya Anga ya "Martyr Muwaffaq Al-Salti," inayojulikana pia kama Kituo cha Anga cha Azraq, ni mojawapo ya vituo muhimu zaidi vya kijeshi huko Jordan.

Kambi hiyo ina shughuli za Jeshi la Anga la Jordan, na katika miaka ya hivi karibuni imepata umuhimu wa kikanda katika suala la maendeleo ya usalama wa Mashariki ya Kati.

Ripoti za kimataifa zinaonyesha kambi hiyo inatumika kwa makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi kati ya Jordan, Marekani na muungano wa kimataifa, huku Jordan ikithibitisha ni kambi ya Jeshi la Anga la Jordan.

Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani katika eneo la Asia (CENTCOM) ilitangaza Jumamosi kwamba wanajeshi wawili wa Marekani wameuawa na wa tatu ametoweka nchini Jordan wakati wakishiriki kuzuia mashambulizi ya makombora ya Iran na ndege zisizo na rubani.

Taarifa kwa vyombo vya habari kutoka CENTCOM ilisema wanajeshi hao wawili waliuawa Ijumaa wakiwa kazini kama sehemu ya operesheni zinazofanywa na vikosi vya Marekani kwa ushirikiano na vikosi washirika kuzuia mashambulizi ya Iran, huku mmoja wa wanajeshi hao akiwa bado hajapatikana.

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran walitangaza Ijumaa kwamba walifanya shambulio la anga dhidi ya meli za mafuta katika kambi ya Azraq huko Jordan.

Jeshi hilo limeeleza wametumia makombora na ndege zisizo na rubani kushambulia maeneo ya kambi hiyo, kulingana na vyombo vya habari vya Iran.

Eneo la kimkakati katika jangwa

Kambi hiyo iko katika eneo la Azraq, takriban kilomita 100 kaskazini mashariki mwa mji mkuu Amman. Eneo hilo linalipa Jeshi la Anga la Jordan uwezo wa kufuatilia sehemu kubwa ya anga ya Jordan na mipaka yake ya mashariki na kaskazini.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kihistoria, kambi hiyo ilianza mwaka 1918, wakati Thomas Edward Lawrence alipotumia Ngome ya Azraq kama kambi ya kijeshi, akilitumia kama eneo la kutua ndege za jeshi linaloelekea kaskazini hadi Daraa wakati wa Mapinduzi Makuu ya Kiarabu. Eneo hilo lina sifa ya mandhari nzuri na hali ya hewa inayofaa kwa kuruka.

1981, iliitwa jina hilo kwa kumbukumbu ya Luteni Muwaffaq al-Salti, aliyeuawa baada ya shambulioa la anga la vikosi vya Israeli Novemba 13, 1966.

Kulingana na Jeshi la Anga la Jordan, Kambi ya Anga ya Muwaffaq Salti ndio kambi kubwa zaidi ya anga nchini Jordan kwa eneo, ina takriban kilomita 35, na inahifadhi wanajeshi wa kivita, matengenezo, usaidizi wa kiufundi na vifaa vya ulinzi wa anga.

Kambi hiyo pia ina kikosi cha ndege za kivita za F-16 kutoka Jeshi la Anga la Royal Jordan, ambazo zimekuwa uti wa mgongo wa Jeshi la Anga la Jordan tangu mwishoni mwa miaka ya 1990 baada ya kuboreshwa hatua kwa hatua kutoka ndege ya Mirage.

Umuhimu wa kambi hiyo hauishii tu na shughuli za ndege za kivita, pia inajumuisha vifaa maalum kwa ajili ya matengenezo na uboreshaji wa ndege za kivita za F-16.

Jeshi la Anga la Jordani linathibitisha kwamba vitengo vya matengenezo ya kambi hiyo vina uwezo wa kufanya matengenezo magumu ya kimuundo na uboreshaji wa kiufundi kwa ushirikiano na kampuni za utengenezaji ndege na mashirika ya kiufundi ya Marekani, jambo ambalo husaidia kudumu kwa shughuli za ndege zao.

Shughuli za muungano wa kimataifa

l

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Picha ya setilaiti inaonyesha ndege za F-15E, A-10 Thunderbolt, na C-130 Hercules katika Kambi ya Anga ya Muwaffaq Salti, huko Al Azraq, Jordan, Februari 2, 2026.

Kambi hiyo imevutia shughuli za kimataifa wakati mapambano dhidi ya "Islamic State" yalipokuwa makali, ripoti za nchi za Magharibi zinaonyesha vikosi vya Marekani viliitumia kambi hiyo kwa shughuli za muungano wa kimataifa wakati huo.

Kambi ya Anga ya Muwaffaq Salti ni mojawapo ya maeneo ya kijeshi yanayohifadhi wanajeshi wa Marekani nchini Jordan kama sehemu ya makubaliano ya ushirikiano wa ulinzi wa nchi hizo mbili.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan Ayman Safadi hivi karibuni alisema kuna wanajeshi wa Marekani nchini Jordan chini ya makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi kati ya Ufalme huo na Marekani.

Ripoti za ulinzi zinaonyesha Jeshi la Anga la Marekani limetumia kambi hiyo kuhifadhi vikosi vya wanajeshi wake wa anga na ndege za kivita na ndege zisizo na rubani katika miaka ya hivi karibuni.

Marekani haijafichua kwa undani shughuli za wanajeshi au vifaa vyote vilivyo ndani ya kambi hiyo, jambo ambalo ni la kawaida katika kambi za kijeshi zinazofanya kazi katika maeneo yenye mvutano.

Katika muktadha huo huo, picha za setilaiti zilizochapishwa na Reuters katika matukio mbalimbali zinaonyesha ongezeko la idadi ya ndege za kijeshi ndani ya kambi wakati wa vipindi vya mvutano katika eneo hilo.