Historia ya siri ya Freemasons iliyopotea

m

Chanzo cha picha, Amanda Ruggeri

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Nadharia nyingi zimekuwa zikienezwa kuhusu Freemasons. Hata hivyo, historia halisi ya chama hicho nchini Scotland, ambayo ilisahaulika na watu wengi kwa karne nyingi, bado imejificha waziwazi mbele ya macho ya watu.

Ikiwa na barabara zilizoezekwa kwa mawe na majengo ya kifahari ya mtindo wa Kijiojia (Georgian), Barabara ya Hill Street ni eneo tulivu katikati ya New Town yenye shughuli nyingi jijini Edinburgh. Ikilinganishwa na kasri kubwa la mji huo au vichochoro vyake vya kale vinavyoonekana vya kutisha, Hill Street haionekani kuwa ni barabara inayoficha siri yoyote.

 Hill Street

Chanzo cha picha, Amanda Ruggeri

Hata hivyo, ukitembea polepole, unaweza kugundua jambo lisilo la kawaida. Juu ya mlango unaozungukwa na nguzo mbili za rangi ya samawati hafifu, kuna maandishi ya dhahabu yanayosomeka: "The Lodge of Edinburgh (Mary's Chapel) No 1."

Juu zaidi ukutani, kwenye jiwe la mchanga lililochongwa, kuna nyota yenye ncha sita iliyoambatana na alama na namba ambazo, angalau kwa watu wasio wanachama wa Freemasons, zinaonekana kuwa za ajabu.

Jengo hilo lililopo namba 19, Hill Street, Mary's Chapel si mahali pa ibada. Ni ukumbi wa Freemasons (Masonic Lodge). Na kwa kuwa kumbukumbu zake zinaanzia mwaka 1599, ndiyo ukumbi wa Freemasons wa zamani zaidi duniani ambao uwepo wake umethibitishwa na ambao bado unaendelea kuwepo hadi leo.

Ukiwa namba 19, Hill Street, tazama juu utaona nyota hii yenye ncha sita, ambayo ni moja ya alama za Freemasons.

Chanzo cha picha, Amanda Ruggeri

Hilo linaweza kuwashangaza baadhi ya watu. Ukiwauliza wengi wanaopenda historia ya Freemasons kuhusu mwanzo wa Freemasonry ya kisasa, watakuambia ulianza mwaka 1717, mwaka ambao kilianzishwa kile kilichokuja kujulikana baadaye kama Grand Lodge of England. Hata hivyo, kwa namna nyingi, Freemasonry tunayoijua leo ni ya Kiscotland kama ilivyo chakula cha haggis au kitambaa maarufu cha Harris tweed.

Kuanzia kipindi cha Enzi za Kati , kulikuwepo vyama vya mafundi wa kuchonga mawe nchini Uingereza na Scotland. Hata hivyo, ni nchini Scotland ambako ushahidi wa kwanza unaonesha kuwa vyama hivyo, au lodge, vilikuwa vinatumika kwa utaratibu wa kudumu.

Kufikia mwishoni mwa miaka ya 1500, kulikuwa na takribani lodge 13 zilizoanzishwa kote Scotland, kuanzia Edinburgh hadi Perth. Lakini ni mwanzoni mwa karne ya 17 ndipo vyama hivyo vya zamani vya mafundi vilipopata mfumo rasmi wa taasisi, hatua ambayo wengi huiona kuwa ndiyo kuzaliwa kwa Freemasonry ya kisasa.

Kwa mfano, kumbukumbu za kwanza za mikutano, ambazo kwa kawaida huchukuliwa kuwa ushahidi bora wa kuwepo kwa mpangilio rasmi wa lodge, zinatoka katika Lodge Aitchison's Haven huko East Lothian, Scotland. Kumbukumbu hizo za Januari 1599 ndizo za zamani zaidi duniani, ingawa lodge hiyo ilifungwa mwaka 1852.

Miezi sita baadaye, mwezi Julai 1599, Mary's Chapel mjini Edinburgh nayo ilianza kuhifadhi kumbukumbu za mikutano yake. Kadiri inavyojulikana, hakuna kumbukumbu za kiutawala kutoka England zinazotokana na kipindi hicho.

"Kwa kweli, hapa ndipo mambo yalipoanza," alisema Robert Cooper, mhifadhi wa Grand Lodge of Scotland na mwandishi wa kitabu Cracking the Freemason's Code.

"Lodge zilikuwa sehemu ya kudumu ya nchi. Na zaidi ya hayo, sasa tunajua kwamba zilikuwa mtandao wa kitaifa. Kwa hiyo, kwa namna fulani, Edinburgh ndiyo iliyoanzisha yote," alisema.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hata kama lodge zilikuwepo mapema zaidi, juhudi za kuupa Freemasonry mfumo rasmi zilianza mwishoni mwa miaka ya 1500.

Mwanamume aliyeitwa William Schaw alikuwa Msimamizi Mkuu wa Ujenzi (Master of Works) wa Mfalme James VI wa Scotland (ambaye baadaye pia alikuja kuwa James I wa England). Kazi yake ilikuwa kusimamia ujenzi na matengenezo ya majumba ya kifalme, kasri na mali nyingine za mfalme. Kwa maneno mengine, alikuwa msimamizi wa mafundi wa kuchonga mawe nchini Uingereza na Scotland.

Ingawa mafundi hao tayari walikuwa na mila na desturi zao, Schaw aliamua kuwa walihitaji mfumo rasmi zaidi wa uongozi. Aliweka kanuni zilizohusu mambo mbalimbali, kuanzia jinsi mafunzo ya wanafunzi wa ufundi (apprenticeships) yanavyopaswa kuendeshwa hadi ahadi kwamba wanachama "waishi kwa upendo na kusaidiana kama inavyowapasa ndugu waliofungwa kwa kiapo."

Mwaka 1598, alituma kanuni hizo kwa kila lodge iliyokuwepo nchini Scotland.

Moja ya masharti yake ilikuwa kwamba kila lodge iajiri mthibitishaji wa kisheria (notary) kuwa karani wake rasmi. Muda mfupi baadaye, lodge zikaanza kuhifadhi kumbukumbu zao za kwanza za mikutano.

M

Chanzo cha picha, Amanda Ruggeri

Hata hivyo, ushawishi wa Scotland ulianza kufifia baadaye. Baada ya kuanzishwa kwa Grand Lodge of England, Uingereza ilichukua nafasi ya kuongoza maendeleo ya harakati za Freemasonry. Na katika karne zilizofuata, asili ya Freemasonry kutoka Scotland ilisahaulika kwa kiasi kikubwa.

"Kwa kuwa Uingereza ndiyo iliyokuwa ya kwanza kuanzisha mfumo wa kitaifa kupitia Grand Lodge, na mfumo huo baadaye ukaigwa na Ireland (takriban mwaka 1725) na Scotland (mwaka 1736), wanahistoria wengi wa Freemasonry nchini Uingereza wamekuwa wakichukulia kuwa Freemasonry ilianzia England na baadaye ikaenezwa duniani kote," anaandika David Stevenson katika kitabu chake The Origins of Freemasonry.

Cooper anakubaliana na mtazamo huo.

"Kwa namna fulani, ni jambo la kushangaza ukizingatia kwamba tuna kumbukumbu zilizoandikwa, na hivyo taarifa za wanachama pamoja na nyaraka nyingine nyingi zinazohusu karibu miaka 420 ya historia ya Freemasonry nchini Scotland," alisema.

"Kwamba kumbukumbu hizo zimeendelea kupuuzwa kama chanzo cha msingi cha historia ni jambo la ajabu sana."

Wakati huohuo, sehemu ambayo watu wengi huihusisha na Freemasonry nchini Scotland ni Rosslyn Chapel, kanisa la enzi za kati linalojulikana kwa michoro na sanamu zake za kuvutia. Baada ya kuchapishwa kwa riwaya ya The Da Vinci Code ya Dan Brown, waongoza watalii wengi wamekuwa wakieleza kuwa michoro hiyo ina uhusiano na Freemasons.

Hata hivyo, uhusiano wa jengo hilo na Freemasonry ni dhaifu na haujathibitishwa kwa nguvu. Hata kitabu cha mwongozo wa kanisa hilo kilichochapishwa mwaka 1774 hakikutaja kabisa uwepo wa uhusiano wowote na Freemasons.

Mary’s Chapel

Chanzo cha picha, Amanda Ruggeri

Inaonekana kwamba historia halisi ya Freemasonry nchini Scotland imefichwa zaidi kuliko kanisa la Rosslyn Chapel ambalo Dan Brown alilifanya lijulikane duniani. Lakini historia hiyo imejificha mbele ya macho ya watu.

Inaonekana katika Grand Lodge na makumbusho yake yanayowakaribisha wageni; katika mhifadhi wa kumbukumbu anayetamani watu wengi zaidi wachunguze nyaraka za kihistoria za shirika hilo; na katika lodge zenyewe, zilizojificha katika kona za barabara na vichochoro vya Edinburgh na miji mingine ya Scotland.

Ingawa milango ya lodge hizo mara nyingi hufungwa kwa watu wasiokuwa wanachama, anwani zao na uwepo wao si siri hata kidogo.