Tanzania inavyochora ramani ya kuvuna thamani ya madini ya kimkakati

    • Author, Yusuph Mazimu
    • Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Karne iliyopita ilitawaliwa na mafuta. Karne hii inatawaliwa na mbio za kupata madini yanayoendesha magari ya umeme, nishati safi, akili mnemba (AI) na teknolojia za kisasa.

Kuanzia Marekani hadi China, kutoka Ulaya hadi Asia, mataifa makubwa yanawekeza mabilioni ya dola kutafuta uhakika wa upatikanaji wa madini yanayojulikana kama madini ya kimkakati. Haya ni madini yanayochukuliwa kuwa muhimu kwa usalama wa kiuchumi na maendeleo ya teknolojia za baadaye.

Wakati dunia ikikimbizana kuyatafuta, Tanzania imeibuka kuwa miongoni mwa nchi zinazovutia macho ya wawekezaji kutokana na uwepo wa madini hayo, yakiwemo Rare Earth Elements, nickel, graphite, cobalt, lithium na heavy mineral sands.

Lakini hoja sio kama Tanzania ina madini hayo. Hoja ni kama taifa hilo litaweza kuyageuza kuwa viwanda, ajira, maarifa na maendeleo yanayoonekana katika maisha ya wananchi wake.

Hazina mpya ya Tanzania

Kwa miaka mingi Tanzania imejulikana duniani kwa dhahabu, almasi na Tanzanite. Hata hivyo, katika kipindi cha hivi karibuni, madini mengine yameanza kupata umuhimu mkubwa kutokana na nafasi yake katika uchumi wa dunia.

Miongoni mwa madini hayo ni Rare Earth Elements yaliyogunduliwa kwa wingi katika maeneo ya Songwe, Ngualla Rare Earth Project, na eneo la Mkiu wilayani Ludewa mkoani Njombe. Madini hayo hutumika katika utengenezaji wa sumaku maalumu zinazotumika kwenye magari ya umeme, mitambo ya upepo na vifaa vya kisasa vya kielektroniki.

Mradi wa Kabanga mkoani Kagera nao umeendelea kuvutia macho ya dunia kutokana na hifadhi kubwa ya nickel, madini muhimu katika utengenezaji wa betri za magari ya umeme.

Kusini mwa Tanzania kuna hifadhi kubwa za mdingi kinywe (graphite), madini yanayotumika katika teknolojia ya betri na mifumo ya kuhifadhi nishati.

Aidha, cobalt, lithium na heavy mineral sands ni sehemu ya rasilimali zinazoongeza uzito wa Tanzania katika ramani mpya ya madini ya kimkakati duniani.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa HakiRasilimali, Adam Anthony, madini hayo ni sehemu ya mabadiliko makubwa yanayoendelea katika uchumi wa dunia.

"Madini haya ni sehemu tu kati ya orodha kubwa ya madini ya kimkakati ambayo ni sehemu muhimu sana katika kutengeneza nishati na pia katika mapinduzi ya kidijitali," anasema.

Kwa nini dunia inayahitaji?

Kadri dunia inavyoongeza matumizi ya nishati safi, mahitaji ya madini hayo yanaendelea kuongezeka. Magari ya umeme yanahitaji betri. Betri zinahitaji nickel, graphite, cobalt na lithium.

Mitambo ya kuzalisha umeme wa upepo inahitaji Rare Earth Elements. Simu za kisasa, kompyuta, mifumo ya mawasiliano na miundombinu ya kidijitali inayotumika katika zama za akili mnemba (AI) nayo hutegemea madini hayo.

"Kwa mfano graphite na nickel hutumika katika betri za kuhifadhi nishati kwenye magari ya umeme. Na kwenye mapinduzi ya kidijitali kuna madini kama cobalt ambayo hutumika katika teknolojia za simu," anasema Adam.

Kutokana na mahitaji hayo, baadhi ya wachambuzi wanaeleza kuwa madini ya kimkakati yana nafasi sawa na ile ambayo mafuta yalikuwa nayo katika karne iliyopita.

Ramani inayochorwa na Tanzania

Wakati mataifa mengi yakijaribu kupata uhakika wa upatikanaji wa madini hayo, Tanzania nayo imeanza kujenga mkakati wake.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, anasema Serikali imeweka mkazo katika madini muhimu na madini mkakati ili kuanzia uwekezaji wake mpaka manufaa yake.

Katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini ilitoa leseni 454 za madini muhimu na madini mkakati, zikiwemo leseni za nickel, cobalt, lithium, heavy mineral sands na Rare Earth Elements.

Hatua hiyo inaonyesha namna sekta hiyo inavyoendelea kuvutia uwekezaji wa ndani na nje.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Uwekezaji Tanzania ya mwaka 2025, sekta ya madini iliendelea kuongoza kwa kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje, ambapo thamani ya mtaji ilifikia dola bilioni 9.79 mwaka 2024 kutoka dola bilioni 8.64 mwaka 2022.

"Ongezeko hili ni matunda ya uhamasishaji wa uwekezaji, mazingira wezeshi kwa wawekezaji, upanuzi wa miradi iliyopo, uwekezaji wa faida zinazozalishwa ndani ya sekta na uunganishaji wa mitaji," anasema Mavunde.

Takwimu pia zinaonyesha kuwa mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 9.1 mwaka 2023 hadi asilimia 10.1 mwaka 2024, huku ukifikia wastani wa asilimia 11.9 katika robo tatu za kwanza za mwaka 2025.

Lakini kwa wataalamu, mtihani mkubwa haupo katika kugundua madini. Upo katika kuongeza thamani ya madini hayo. Kwa miongo mingi, nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikiuza malighafi huku sehemu kubwa ya thamani ya kiuchumi ikibaki nje ya mipaka yake.

Ndiyo maana Serikali imekamilisha Mkakati wa Uongezaji Thamani Madini unaolenga kuhamisha sekta kutoka kuuza madini ghafi kwenda kuuza bidhaa zenye thamani kubwa zaidi.

Serikali pia inaendelea na ujenzi wa kituo cha jiolojia kitakachotoa mafunzo na huduma za kitaalamu katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini.

"Kwenye mjadala wa sasa, jambo kubwa si kuchimba tu. Ni kuangalia nchi za Afrika zenye madini kama haya zinawezaje kuongeza thamani badala ya kusafirisha malighafi," anasema Adam Anthony.

Je, wananchi watanufaika?

Kwa watanzania hili ndilo swali kubwa kila ugunduzi wa madini ukitangazwa. Kwa wananchi wengi, mafanikio ya sekta ya madini hayatapimwa kwa ukubwa wa hifadhi zilizopo ardhini. Yatapimwa kwa matokeo yanayoonekana katika maisha yao. Paul Libesa wa Geita anasema matarajio yake ni kuona rasilimali za nchi zinageuka kuwa manufaa ya wananchi.

"Mimi nalia sana na manufaa. Madini yatunufaishe. Tumepewa rasilimali, tuzilinde na zitusaidie kubadilisha maisha yetu."

Waziri wa Madini, Mavunde, anasema Serikali inatambua umuhimu wa kuhakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali hizo.

"Serikali itahakikisha Watanzania wananufaika na madini mkakati na madini muhimu," anasema.

Mkurugenzi wa Hongji Mining Co. Ltd, Yahya Mohamed, inayofanya utafiti wa Rare Earth Elements huko Njombe inasema wao ni wadau wanaoangaliwa na wananachi kwenye eneo la ajira, fursa za biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi wa eneo hilo.

"Tunataka kuona wananchi wa Njombe wanakuwa sehemu ya mafanikio ya mradi huu kupitia ajira, fursa za biashara na ongezeko la mapato ya kiuchumi," amesema Mohamed.

Kwa upande wake, Rahel Mayala wa Shinyanga anaamini sekta ya madini inaweza kubadili maisha ya Watanzania wengi zaidi ikiwa ajira na fursa zitanufaisha wananchi.

"Nimewahi kufanya kibarua kwenye mgodi wa Resolute miaka ya nyuma. Najua nimejenga na nimesomesha watoto wangu wote kutokana na kazi hiyo. Wahakikishe ajira ni za Watanzania na kinachopatikana kinufaishe Mtanzania."

Katika dunia inayokimbilia nishati safi na teknolojia za kisasa, Tanzania imepewa nafasi ambayo si kila taifa limeipata. Chini ya ardhi kuna madini ambayo dunia inayahitaji na yanaweza kuwa msingi wa kujenga uchumi wa Tanzania wa karne ya 21.